Watanzania wanapaswa kumpokea Rais Bush kwa mabango
Raphael Mgaya
HAKUNA shaka ukweli ni nguvu! Ni silaha dhidi ya uongo. Katika kila jamii, tangu kale, tabaka tawala huhodhi vyombo vya habari na njia zozote za kusambaza taarifa ili kulinda mfumo uliopo.
Mfumo wa kihafidhina, kandamizi na nyonyaji hutumia vyombo vya habari kueneza uongo na propaganda ili kudanganya umma na kudumaza harakati za kupambana na tabaka tawala.
Hadi tu umma utakapopata fursa ya kupata mawazo na taarifa sahihi, ndipo utakapogeuka na kuwa nguvu itakayoweza kuleta mapinduzi yatakayoung'oa mfumo uliopitwa na wakati na kandamizi uliopo madarakani!
Nimesoma taarifa kuhusu ujio wa Rais wa Marekani nchini Tanzania na nchi nyingine za Afrika. Nimesoma pia taarifa ya John Chiligati, Katibu wa Itikadi ya Uenezi wa CCM, ikidai kuwa "ziara hii tuitumie kuimarisha uhusiano wetu na Marekani, wananchi wajiandae katika ugeni huu mkubwa".
Chiligati ametoa pia takwimu ya misaada ya kifedha ambayo Marekani imeisaidia Tanzania, ambao ukiziangalia kwa juu juu, bila kuzingatia masuala mengine muhimu, Watanzania wengi bila shaka watadhani Marekani au Rais Bush ni msamaria mwema!
Taarifa ya CCM, inaonyesha namna ambavyo tabaka la mabwanyeye ndani ya nchi (national bourgeois class) linavyoshirikiana na mabwanyeye wa kimataifa (international bourgeoisie) katika kuendeleza unyonjaji wa umma na mali za nchi zilizonyuma kiuchumi kwa masilahi ya ubepari.
Lengo la taarifa ya CCM ni kuwapotosha Watanzania kutoka kwenye masuala nyeti yanayohusu ukombozi wao na badala yake wajishughulishe na namna ambayo watamfurahisha Bush ili awaongezee misaada!
Katika nchi nyingi anakotembelea Rais Bush, anakutana na upinzani mkali sana kutoka kwa wanachi, si watawala. Mwaka jana Bush alipotembelea Marekani ya Kusini, alikutana na upinzani wa kihistoria kutoka kwa wananchi wa Venezuela, Argentina, Brazil, n.k.
Wanachi wa Marekani ya Kusini walitumia fursa zao kumwabia Bush ukweli. Walimpokea kwa mabango wakisema 'komesha ubeberu wa Marekani', 'Komesha vita vya mafuta', 'funga jela ya Guantanamo' n.k.
Wakati Bush akipambana na upinzani mkali, Hugo Chavez, mwanamapinduzi, Rais wa Venezuela, alipokewa kwa shangwe za vigelegele na milio ya risasi na mamilioni wanachi kokote alikokwenda Amerika ya Kusini kama ishara ya kumuunga mkono katika harakati zake za kukomesha ubepari na ubeberu wa Marekani duniani.
Hakuna nchi inayoweza kuendelea kwa misaada duniani. Hata historia imeonyesha kuwa nchi zote zilizoendelea, zimeendelea kwa kutumia rasilimali zilizopo ndani ya nchi, ardhi, madini, maji, misitu n.k. kwa kutumia teknolojia, ujuzi na elimu iliyopo.
Hata Mwalimu Nyerere alituasa kuwa jamii haiwezi kuendelezwa, bali inaweza kujiendeleza yenyewe! Misaada ambayo Marekani inaipa Tanzania haina maana kabisa ikilinganishwa na taabu, adha na mateso ambayo Watanzania na watu wengi duniani wayapata kwa sababu ya dhuluma za ubeberu wa Marekani na washirika wake!
Kwa bahati mbaya, tofauti na sehemu nyingi duniani, Afrika tuko nyuma katika utashi wa kisiasa na hali halisi ya mambo duniani kutokana kwanza na watawala wetu na pili kutokana na historia yetu.
Ndiyo maana, wengi hawajui dhuluma ya Marekani duniani. Na kwa mantiki hiyo, taarifa ya CCM, inaweza ikawafanya Watanzania wengi kumpokea Bush kama mkombozi, na si vinginevyo! Ni kwa sababu hiyo hiyo, nina wasiwasi kuwa upinzani alioupata Bush sehemu nyingi duniani anaweza asiupate Afrika.
Mataifa mengi yanashindwa kuendelea kwa sababu ya mfumo wa kinyonyaji uliopo duniani. Marekani ndilo taifa linalohodhi mfumo huu na linatumia gharama kubwa kuhakikisha linaulinda.
Moja ya misingi ya mfumo huu ni biashara huria. Biashara huria ni moja ya sababu za kufukarishwa kwetu. Shirika la Biashara Duniani (World Trade Organisation-WTO) linaruhusu nchi tajiri kilinda masoko yake dhidi ya bidhaa rahisi kutoka nchi masikini ambazo nyingi ziko Afrika.
Kwa kufanya hivi nchi maskini hazipati masoko ya bidhaa zao za kilimo, nguo, n.k ambazo ndio msingi wa maendeleo. Kwa upande huo huo nchi maskini zinalazimishwa kufungua mipaka yako kuruhusu bidhaa kutoka nje, matokeo yake ni kuwa nchi masikini zimekuwa masoko ya nchi tajiri.
Hali kadhalika, nchi tajiri zinatoa ruzuku kwa wazalishaji wake na matokeo yake ni wazalishaji hawa kuzalisha bidhaa ambao zinauzwa bei ya chini katika soko la dunia huku bidhaa kutoka nchi masikini zikishindwa ushindani kwa kuwa bei yake ni kubwa kwa sababu ya gharama za uzalishaji.
Kwa maneno mengine hakuna haki katika biashara huria. Kwa mujibu wa taarifa ya UNCTAD - Tume ya Umoja wa Mataifa ya Biashara na Maendeleo - kama vikwazo hivi katika biashara vingeondolewa, nchi masikini zingeongeza kipato kwa dola la Marekani billioni 700 ambazo ni sawa na mara 13 ya misaada yote ya maendeleo duniani kwa mwaka!!
Kama unyonyaji huu ulioletwa na WTO ungekomeshwa, umasikini ungekuwa umepungua sana duniani, badala ya kuongezeka kama ilivyo leo.
Aidha, licha ya upinzani mkali duniani kote, Rais Bush aliivamia Iraq mwaka 2003 ili kudhibiti uzalishaji wa mafuta na Usambazji wa mafuta Iraq. Vita vya Iraq vimegharimu maisha ya watu takribani laki saba (700,000).
Hali ya Iraq si shwari, watu wengi wanaendelea kupoteza maisha, vita vimeacha yatima, wajane na walemavu kwa maelfu. Kudhilisha dunia ubabe wake, mshirika wake, Tony Blair (Waziri Mkuu mstaafu wa Uingereza, aliyemuunga mkono kuivamia Iraq) sasa ameteuliwa kuwa mshauri wa Benki ya J. P. Morgan, Benki ya Marekani ambayo imepewa jukumu la kuiendesha Benki Mpya ya Iraq!
Hapa inaonyesha jinsi tabaka tawala linavyoshirikiana na tabaka la kibepari katika kuendeleza masilahi ya ubepari na ubeberu wa Marekani.
Maovu ya Marekani ni mengi, si rahisi kuyaeleza yote katika ukurasa huu,. Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) ndiyo lililosababisha Nelson Mandela kutiwa mikononi mwa makaburu na hatimaye kuishi miaka 27 gerezani! Donald Richard aliyekuwa ofisa wa CIA Afrika ya Kusini, akijifanya ofisa balozi mjini Durban, akawataarifu polisi wa makaburu mahali ambako wengemkuta na kumkamata Mandela. Ikimbukwe pia kuwa, Bush (Mkubwa) alikuwa ndiye Afisa Mkuu wa CIA kipindi hicho!
Ni Marekani inayojitia kutoa misaada ya ukimwi ambayo iliongoza makakati wa mataifa ya Magharibi ya kuzuia ulegezaji wa masharti ya sheria ya hati miliki (Trade Related Intellectual Property Rights) ili kuziwezesha nchi masikini kuanzisha viwanda vya kutengeneza madawa ya kupunguza makali ya ukimwi.
Marekani kwa kushirikiana na Ubelgiji wanadaiwa kumuua Patrice Lumumba, Waziri Mkuu wa Kwanza wa Kongo sasa DRC na kumweka madarakani dikteta Mobutu Sseseko. Marekani ndio taifa lililo mstari wa mbele katika kuisaidia kwa moyo, kifedha na kwa kuipa silaha Israeli katika mpango wake wa kuwakandamiza Wapalestina.
Ni Marekani inayochafua mazingira kwa kiasi kikubwa duniani, taifa ambalo limekataa kuridhia itifaki ya Kyoto inayohusu kuzuia uchafuzi wa mazingira.
Licha ya maovu yote ya Marekani, bado watawala wetu wanazidi kujikomba kwa Marekani? Inakuwaje Kikwete mara baada ya kuchaguliwa kuwa rais, haraka haraka alikwenda kwa Bush, eti kujitambulisha? Inakuwaje baada ya kampeni baadhi ya wanasiasa wanakwenda kwa Bush na wanaporudi wanaeleza Bush amewasifu kuwa wamefanya kampeni vizuri?
Nalazimika kuamini kuwa watawala wetu wanamtazamo na uelewa finyu kuhusu hali halisi ya mambo duniani. Mwalimu Nyerere alikuwa mkali kwa kuwa alikuwa akijisoma sana, hivyo alipata kujua hali halisi ya mambo duniani. Watawala wetu leo nadhani hawasomi, kazi yao ni ziara za kuzunguka tu kama wanyapara.
Afrika ndilo bara pekee linalozidi kuwa masikini wakati mataifa mengine yanazidi kuendelea, tusipojihadhari tutaendelea kuwa nyuma milele.
Ni wakati wetu sasa wa kukasirika na kuamka na kusema sasa basi, tumechoka na watawala mamluki na manyapara. Na kwamba hatutaki kuendelea kunyonywa na mataifa ya kibepari. Inawezekana kuwa masikini na ukaheshimika.
Ningelikuwapo Tanzania wakati wa ujio wa Rais Bush ningeliandamana (hata peke yangu) kumpinga. Lakini, nadhani Watanzania wanapaswa kuniunga mkono, viongozi wa nyama vyote vya siasa pamoja ikiwamo CCM. Viongozi wa NGO hamasisheni wananchi wajitokeze kumpokea Bush kwa mabango ya kuwalilia yatima na wajane wa Iraq, kuwalilia wagonjwa na yatima wa ukimwi, kujililia wenyewe kwa sababu ya umasikini uliopandikizwa na Marekani na mataifa mengine ya kibepari na kupinga uchafuzi wa mazingira.
Watanzania, tumieni fursa hii kumweleza Bush kuwa misaada anayoipa Tanzania anarudisha sehemu ndogo tu ya kile anachotuibia sasa na kile ambacho mababa zetu wa kale waliochukuliwa kama watumwa walikizalisha!
Mwandishi wa makala hii ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Warwick, Uingereza.
Anapatikana kwa Barua pepe: b.t.mgaya@warwick.ac.uk
No comments:
Post a Comment