]
Na Hassan Abbas
NI wazi kuwa msomaji wangu makini hasa wale wanaofuatilia sana safu hii watashangaa kwa nini leo nakasirishwa na kukasirika kwa Rais? Mshangao huo utakuwa mkubwa zaidi kwa wale ambao walisoma makala yangu iliyokuwa na kichwa cha habari "Rais Kikwete:Haya ndiyo maslahi ya taifa." Katika makala hiyo nililidadavua sakata la mabilioni yaliyopotea Benki Kuu na kwenda mbali zaidi ya kumpongeza Rais kwa kuchukua uamuzi mzito, niligusia haja ya yeye kwenda mbali na kuhakikisha mabilioni hayo yanarejea kwa wananchi. Ni katika eneo hili la namna tulivyoanza mchakato wa kufikia lengo la kuwafikisha katika vyombo vya kisheria wahusika, ndipo leo imenilazimu kuuweka kizimbani muelekeo wa Rais na 'kamati' aliyoiunda inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kwanza kabisa tuliambiwa, kama ambavyo kijitabia hiki kilivyoanza kushamiri, kwamba Rais alikasirishwa sana na 'madudu' katika ripoti ya BoT ambayo hata sasa haijawekwa bayana. Nikimnukuu Katibu Mkuu Kiongozi, Bw. Phillemon Luhanjo, alisema hivi katika 'kidesa' chake kinachofupisha yale uchunguzi wa Ernst And Young ulichokibaini: " Baada ya kupitia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali na Mkaguzi wa Nje, yaani, kampuni ya Ernst and Young. Mhe. Rais amesikitishwa na kukasirishwa na taarifa ya kuwepo vitendo vya ukiukwaji wa makusudi wa sheria, kanuni na taratibu za madeni ya nje vilivyofanywa katika taasisi muhimu na nyeti katika Benki Kuu." Kwa mujibu wa nukuu hiyo Rais, hakufurahishwa hata kidogo na wizi huo tena, kwa msisitizo, narejea neno 'wa makusudi' uliofanyika BoT.Lakini nukuu hiyo pia inaweka rekodi ya kuwa ya pili kwa wasaidizi waandamizi wa Rais kuuarifu umma hasira za kiongozi wetu. Nitaomba samahani kwa wasomaji wangu, kwamba leo katika kukasirishwa kwangu na kukasirika huko kwa Rais, nitakuwa mwanataaluma sana wakati fulani, lengo likiwa moja tu; kuhakikisha tunaeleweana vyema. Kwa ujumla nimestushwa na kasirika ya Rais jinsi inavyotafsiriwa kivitendo. Katika hilo la kamati ambayo ndiyo inatafsiri kivitendo kasirika ya Rais, kuna masuala mawili yanaonesha huenda tukaishia kwenye usanii na bilioni 133 zilizofujwa zikapotea kabisa au tukajikuta mwisho wa siku tumetumia bilioni 140 katika mchakato wa kutaka kuziokoa bilioni 133! Nasema hivi kwa nini? Mosi, muda ambao 'tume' hiyo imepewa; miezi sita unatia shaka! Pili mbinu zilizoanza kutumiwa na 'tume' hiyo; kuanza kukusanya maelezo ya wenye taarifa zozote kuhusu BoT nazo ni ngeni kabisa katika taaluma ya sayansi ya makosa ya jinai. Kwa nini natofautina sasa na Rais na watu hawa wa 'tume' hiyo. Hoja yangu ya kwanza ni kwamba kwanza ni hatari sana kumpa muda adui yako. Hili Rais Kikwete analifahamu kwa kuwa amesoma sayansi za kijeshi, mimi nilizigusa tu katika pitapita zangu za 'kukimbia umande.' Zaidi si tu kivita, bali katika hali halisi, kisheria ni jambo la hatari sana kama utampa mtuhumiwa nafasi ya kujua unakuja na kesi gani, una ushahidi gani, unautoa wapi na lini ndio utashtaki.Ndio maana kuna mamia ya watuhumiwa wanakataliwa dhamana kwa sababu tu akiwa mtaani anaweza kupata mwanya wa kuharibu ushahidi muhimu. Katika hili napata wasiwasi sana kama kuna nia ya dhati ya kufika kila Mtanzania anakotaka tufike katika hili, naanza kuhisi sanaa na usanii vitatawala katika suala hili. Mwanasheria Mkuu, Johnson Mwanyika, Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema na Mkurugenzi wa TAKUKURU, Dkt. Edward Hosea ni miongoni mwa wajumbe wa 'kamati' hiyo ambao pia wote kwa bahati nzuri ni wanataaluma wazuri wa sheria. Hao kwa taaluma zao, kama watauweka kando usanii, wanafahamu fika kuwa kesi ya BoT ni ya kihistoria katika taifa hili na ni kesi inayowahusisha watu wenye utaalamu katika maeneo walikotuhumiwa kuchota fedha na zaidi ni kesi ambayo hata hao watuhumiwa watataka waonekane wasafi mbele ya jamii; hawatakubali kufa kibudu. Ni kwa jinsi hii, nilidhani, na kwa hakika sheria zinaruhusu, kama inavyotokea kwa kesi nyingine za jinai, baada ya Rais kupatiwa ripoti kamili, wataalamu wake wa sheria wangeipitia na kuona kama kuna kesi ya msingi, kitaalamu wanaita prima fascie case. Kwa hakika kwa mujibu wa Luhanjo kama tulivyomnukuu hapo juu, katika suala la BoT kuna prima fascie case na ndio maana maneno kama 'kwa makusudi walikiuka sheria, kanuni na taratibu,' yametumika kwenye nukuu tuliyoiona hapo awali. Kwa mujibu wa utaalamu wangu mdogo wa sayansi za makosa ya jinai, kosa la jinai linapande kuu mbili ili likamilike; ile ya nia ovu (malice aforethought au malice prepence) na kitendo kamili cha kufanya jinai husika (actus reus). Bila kuingia ndani katika ripoti ya ukaguzi wa BoT, kwa ile karatasi tu yenye kurasa nane aliyoisambaza Bw. Luhanjo kwa wanahabari, ni dhahhiri kuwa makosa kamili ya jinai yametendeka BoT; kwanza ripoti imebaini 'kwa makusudi kanuni na sheria zilivunjwa.' Neno hili linaashiria kuwepo nia ovu. Na kwa kuwa ripoti imebaini kuwa sh. bilioni 133 zilifunjwa na imeyataja makampuni kadhaa yawe feki au ambayo yapo kihalalim lakini yalitumia 'njia za panya,' kupata fedha hizo tayari actus reus imetimia. Kosa kamili hapo la jinai limekamilika kutendeka. Kinachofuata kwa elimu yangu ya kabwela ni Je, kama kuna kosa la jinai limetendeka, ni lipi au ni yapi kwa kadiri ya ushahidi ambao Ernst And Young wameuambatanisha katika ripoti yao? Na swali lingine la msingi ni Je, akina nani wanahusika? Kulijibu hili nalo tunarudi pale pale kwenye nukuu ya Bw. Luhanjo, alipokiri kulikuwa na 'uvunjaji wa makusudi wa sheria.' Kama Ernst And Young walibaini uvunjaji wa makusudi, basi wanawajua au wamewataja wavunjaji hao wa makusudi. Na hata kama hawajatajwa, kitu ambacho siamini, basi kwa kupitia rejea ya nyaraka zilizoko, waliohusika kuzisaini au kuziidhinisha na watendaji wengine wote wanaohusika na mchakato wa uendeshaji wa akaunti ya EPA ni watu wa kwanza kisha wanafuatia wakurugenzi wote za zile kampuni zilizotajwa. Maswali hayo hapo juu ukimpa mtu aliyehitimu vyema darasa la Criminal Law la Profesa Ibrahim Juma, Criminal Procedure la Profesa Sifuni Mchome na Profesa Abdallah Saffari au darasa la Legal and Statutory Interpretation la Professor Issa Shivji, Administrative Law la Prof. Jwan Mwaikyusa au darasa adhimu la sheria za madhara (Torts) la Dkt. Asha-Rose Migiro, Dkt. Michael Wambari na Profesa Pallamagamba John Kabudi, kwa uchache tu, haiwezi kumchukua zaidi ya wiki kukakabidhi aina ya mashitaka yanayofaa kufunguliwa. Lakini pamoja na ushahidi mzito wa nyaraka ambao ni lazima umeambatanishwa kwenye ripoti (rejea dokezo kuwa baadhi ya risiti zilizowasilishwa na makampuni hayo BoT zilikuwa feki, kuonesha kuwa ripoti inaviambatanishi kama hivyo au vinaweza kupatikana, kama havijaambatanishwa). Na kama kuna viambatanishi vya nyaraka katika ripoti ya Ernst and Young basi tunataka ushahidi gani mzuri zaidi ya huo? Au tusema Tanzania imejivua kufuata sheria za kiingereza? Maana kama tunafuata mfumo wa sheria za kiingereza, kitaalamu mpaka sasa ushahidi bora zaidi duniani ni ule wa nyaraka yenyewe (Rejea shauri mashuhuri la Kiingereza la Omychund v Barker (1745) 1 Atk, 21, 49; 26 ER 15, 33, tazama falsafa ya Lord Harwicke katika hukumu hiyo). Inashangaza kuona kampuni yenye wataalamu imefanyakazi kitaalamu, halafu leo tunaanza kukwepa hoja na eti tunaalika wananchi wenye taarifa wazitoe. Zipi zaidi ya hizi za Ernst And Young? Ushauri wangu wa kitaalamu katika hili ni kwamba hakuna hoja wala haja ya kuuma maneno na kuwaachia wananchi zigo la 'mnyamwezi walibebe,'Hiyo ilikuwa kazi ya Ernst And Young ambayo kwa hakika wameitimiza vyema. Ni mwananchi gani ana uwezo, urahisi na fursa ya kujua taarifa za jikoni kama Benki Kuu zaidi ya vyombo vya Serikali yenyewe; wanausalama wa taifa, mafisadi wenyewe popote waliko na wafanyakazi wazalendo wa ndani ya BoT ambao tunajua walijitolea sana wakati wa uchunguzi wa kampuni ya Ernst and Young kueleza walichokijua? Huu 'uchunguzi' mwingine unaofanywa kwa kualika wananchi ambao tayari wana misongo mingine ya kimaisha, eti watoe taarifa, wakati kuna wataalamu tuliowaalika na kuwalipa mamilioni watufanyie kazi na wengine wapo nchini wanaendeleea kulipwa kila mwezi. Hii ni kuzidi kuibua maswali magumu juu ya kiwango cha kukasirika kwa Rais. Wakati watanzania wakitafakari kukasirika huko kwa Rais na watu kama sisi tukiamua kukasirikia kukasirika huko kwa Rais, wengi hawajasahau rejea ya msingi ambayo inapaswa kutosahaulika katika nchi hii na sisi tunaokumbuka ya nyuma katika kuangalia yaliyopo na kuakisi yajayo, hatujaisahau. Rais Kikwete alipopokea ripoti ya uchunguzi juu ya mauaji ya wafanyabiashara wa Mahenge, Morogoro (waliotuhumiwa kuwa majambazi), ndani ya saa 48 tu mtuhumiwa mkuu, Bw. Abdallah Zombe alikamatwa na wenzake (wakati uchunguzi ukiendelea). Mafisadi wa BoT nao, ili, kama nilivyogusia, wasipate nafasi ya kufanya ufisadi zaidi, hawakupaswa kupewa muda, wangechukuliwa hatua za haraka kama ilivyokuwa kwa akina Zombe, wakati uchunguzi unaendelea, hilo sheria inaruhusu. Lakini sasa miezi sita hii inaibua maswali magumu na kwa hakika watawala wetu wanalazimika kupanda kizimbani, kizimba cha hoja kujibu: Miezi sita yote hii ya nini? Kwa maoni, ushauri: simu 0713 584467
No comments:
Post a Comment