Friday, 15 February 2008

MAHOJIANO YA MWANYIKA NA KAMATI YA RICHMOND

Mwanyika mbele ya Kamati ya Richmond Mwandishi Wetu Februari 13, 2008 Raia MwemaMWISHONI mwa mwaka jana, Spika Samuel Sitta, aliunda Kamati Teule ya Bunge kuchunguza zabuni iliyotolewa kwa Kampuni ya Richmond Development ya kuzalisha umeme wa dharura. Kamati hiyo iliongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harisson Mwakyembe. Wajumbe wake walikuwa ni mbunge-CUF Habib Mnyaa na wabunge wa CCM: Stela Manyanya, Lucas Selelii na Herbert Mtangi. Raia Mwema wiki hii imefanikiwa kupata nakala ya mahojiano ya Kamati na mmoja wa mashahidi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika.
Mahojiano na mashahidi wengine yatachapishwa kwa kadri yatakavyopatikana.
Dk. Harrison Mwakyembe: Mheshimiwa (Mwanasheria Mkuu) AG, baada ya Richmond kuelekea kushindwa kutekeleza majukumu yake, TANESCO ilitoa default notice kwa Richmond, tunayo barua hapa. Tulitaka kujua ni nani aliyei-convince TANESCO isiendelee na intention (nia) yake ya kuvunja huo mkataba na badala yake kazi hiyo ikawa assigned (ikapelekwa) kwa Dowans.
Johnson Mwanyika: SijuiDk. Harrison Mwakyembe: Ofisi yako haikushiriki katika mchakato huo?Johnson Mwanyika: Sina habari hiyo.
Dk. Harrison Mwakyembe: Kifungu cha 15 (12) cha makataba ambao mlishiriki kuutengeneza kati ya Richmond na TANESCO, kinataka assignment yoyote ifanyike kwa mutual agreement kati ya TANESCO na Richmond; Je, ushiriki wenu katika hili ulikuwaje, maana ni suala la kisheria?
Johnson Mwanyika: Labda kwa sababu Ofisi yangu ni kubwa, mimi ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali lakini pia nina wakuu wa Idara. Kwenye sehemu kama hizo ambazo unazungumzia, kuna mkuu wa madai ambaye mara nyingi anashughulika na mambo kama hayo. Inawezekana kabisa labda Wizara ya Nishati iliomba ushauri kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, inawezekana. Lakini mimi binafsi kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kama Mwanyika, halikunifikia hilo.
Dk. Harrison Mwakyembe: Sasa unaweza kutusaidia afisa ambaye anaweza kuwa ame-handle masuala kama hayo ili aweze kuisaidia Kamati?
Johnson Mwanyika: Afisa ambaye anashughulikia masuala kama haya ya nishati katika ofisi yangu ya Mwanasheria Mkuu ni Chidowu.
Dk. Harrison Mwakyembe: Ambaye pia amekuja kwenye Kamati na masuala mengi alikuwa anakusukumia wewe, akisema utayajibu.Johnson Mwanyika: Kama lipi alinisukumia?
Dk. Harrison Mwakyembe: Tutamrudia tena kwa sababu tulimwambia tukimhitaji tutamwita tena, awe tu na, kwanza una imani naye kubwa.Swali jingine ambalo pengine lilikufikia, ni masuala ya kisheria tu kwa sababu inaonekana mkataba huu umekuwa na maswali ambayo mengi yanatokana na udhaifu katika negotiation na vile vile katika drafting. TANESCO imeingia mkataba na kampuni inayoitwa Richmond Development Company LLC ya Marekani lakini Marekani hakuna kampuni ya aina hiyo. Sasa washauri wako, walishindwaje ku-notice kitu hicho? Sisi tumeshindwa kabisa kuipata kampuni inayoitwa Richmond Development Company LLC Houston, hakuna kabisa!
Johnson Mwanyika: Kama unavyofahamu, sisi tunaingia kwenye mambo ya mikataba much later, mambo ya kutafuta mtu yeyote ambaye wanaingia naye mkataba, ni juu ya procurement entity na ni juu ya Accounting Officer. Wakishamaliza mazungumzo na huyu mtu, ndiyo wanatuletea sisi barua kutueleza kwamba, kuna mambo kama haya ambayo yametendeka. Kwa hiyo, wanatushauri sisi tuweze kuwatayarishia mkataba. Kwa hiyo, whether or not kulikuwa na huyu Richmond LLC, watu ambao wanaweza kujua ni Wizara ya Nishati na Madini.
Stella Manyanya: Mheshimiwa mwenyekiti, mimi naomba unisaidie kidogo. Kwa sababu ya uelewa wangu mdogo wa sheria, napatwa na tatizo juu ya mipaka ya shughuli zetu katika Serikali kuhusu huyu Accounting Officer, ambaye pengine kiutaalamu, anaweza kuwa ni mtu wa aina tofauti kabisa na sheria na juu ya Mwanasheria ambaye nilifikiria ndiye wa msaada au consultant wa masuala ya kisheria katika department kama hizo. Sasa katika hili, unatuambia kwamba masuala yote yanayohusu utafiti wa kisheria, ambayo labda yangetumika kuweza kutambua kama hii kampuni iko kule au haiko, yalikuwa hayahusu kabisa kupata msaada kutoka kwa Mwanasheria wa Serikali?
Johnson Mwanyika: Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu langu ndiyo hilo kwamba sisi kazi yetu ni kutayarisha mikataba kama tutaombwa na wizara zinazohusika. Mazungumzo ya namna ya kumpata huyo mtu wanayetaka kuingia naye mkataba ni wizara yenyewe, ndiyo inayohusika. Mwanasheria Mkuu wa Serikali kazi yake ni kushauri kisheria tu kama ataombwa na Wizara zinazohusika, lakini whether huyo mtu alikuwapo au hakuwapo ni juu ya hawa ambao walimtafuta wakampata, wao ndio wanaopaswa kujua kwamba yupo au hayupo, yupo wapi. Sisi wakati tukiangalia mkataba, tunaangalia capacity kutokana na maandishi yaliyoko pale.Je, huyu mtu ana capacity ya kuingia mkataba? Kama tukiridhika kwamba ana capacity ya kuingia ndiyo tunaendelea. Je, kuna muhtasari wa bodi yao kuzungumzia juu ya huo mkataba ambao tunapaswa sisi tutayarishe? Tukiona upo ndiyo tunaendelea na shughuli ya kutayarisha mkataba huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala hili ambalo mnalizingumzia sasa hivi, nilipozungumza na mtaalamu wangu ambaye alikuja kutoa ushahidi mbele yenu, alinihakikishia kwamba, vitu vyote hivi vilikuwapo. Kulikuwa na resolution ya bodi ya Richmond kuhusiana na mkataba huu, vitu vyote hivi waliviona.
Dk. Harrison Mwakyembe: Bahati mbaya, mtaalam tulikuwa naye hapa, tulijaribu hata kumwuliza, maana katika maelezo yake, moja ya sababu kubwa iliyofanya Richmond kupewa mkataba ni ushiriki katika hii zabuni, pamoja na kampuni popular inayoitwa Pratt and Whitney. Sasa tukasema kwa sababu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ndiyo advisor mkuu wa mambo ya sheria, ndio tukamwuliza yeye alihakikishaje kwamba Pratt and Whitney na Richmond wana uhusiano wa kisheria? Akatuonyesha mkataba fulani ambao ni ku-share information lakini wa kushirikiana katika ku-execute project yoyote, tukio ambalo ni weakness kubwa pengine hata katika ku-interpret huu mkataba wenyewe.
Johnson Mwanyika: Mheshimiwa Mwenyekiti labda kwa sababu record zilizoko kule ofisini zinaonyesha wazi kwamba huyu Richmond pamoja na huyo Pratt, kuna mtu wao alihusika kabisa katika negotiation juu ya mkataba huu, watu wa Nishati wanamtaja kwa jina. Ukiangalia minutes za vikao vile ambavyo wamekaa kabla ya kuingia huu mkataba, zinaonyesha wazi kwamba kuna mtu wa hiyo kampuni ambaye alishiriki katika majadiliano.
Dk. Harrison Mwakyembe: Kwa nyaraka tulizonazo, huyu hakushiriki, kilichokuwapo ni business card feki tu.Johnson Mwanyika: Wakati fulani wanasema kulikuwa na video conference kati ya hiyo Negotiation Team na huyo Pratt huko Marekani. Ndivyo walivyosema, kufuatana na minutes zilizoko kwenye mafaili ofisi zetu.
Stella Manyanya: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kama ulivyosema kwamba, mengi uli-delegate kwa watu ambao wangefanya, kwa hiyo, tunachohitaji kwako hasa ni kutaka kufahamu zaidi.Kwa mfano, nimeona mahali kuna abbreviation za RDEVCO ikiwa imesajiliwa kama kampuni na sehemu nyingine nikaona kuna kitu kinachoitwa Richmond Development Company LLC; je, ile abbreviation ni lazima iwe hiyo kama hakujawa na definition ambayo imeelezwa mahali popote pale?
Johnson Mwanyika: Mheshimiwa Mwenyekiti kama nilivyosema awali, katika negotiations kulikuwa na Kamati Maalum, ambayo iliteuliwa iliyoitwa Government Negotiation Team. Wao ndio walishiriki katika negotiations pamoja na huyo Richmond. Kwa hiyo, hao watu ndio wanaweza kujibu maswali yote haya ambayo mnaniuliza, lakini mimi as Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mambo ya negotiation sikushiriki kabisa.
Herbert Mtangi: Mheshimiwa AG, tunakuomba utusaidie kwa sababu swali lililokuwa limeulizwa hapa ni la kutaka opinion yako wewe kama AG ili kuisaidia Kamati. Kwa mfano, tunafahamu TANESCO kama TANESCO ikiandikwa vile TANESCO ni kifupi cha Tanzania Electric Supply Company, lakini bila kupewa tafsiri ya shirt form hii, nikikuta mahali pameandikwa TANESCO na mahali pengine pameandikwa Tanzania Electrical Supply Company Limited, hivi kutakuwa na dosari nikisema hizi ni entities mbili tofauti
Johnson Mwanyika: Mheshimiwa Mwenyekiti, inategemea vitu vingi, inawezekana mtu ana makosa ya kuandika hivyo, lakini ambao wanaweza kujibu swali hilo vizuri ni watu wa Wizara ya Nishati na Madini, ambao ndio walihusika tangu mwanzo katika kushughulikia suala hili la kutafuta mwekezaji wa kutupatia jenereta kwa ajili ya kuzalisha umeme wakati ule wa dharura.
Herbert Mtangi: Ni kweli tunaweza tukajibiwa hilo na watu wa Wizara ya Nishati na Madini, lakini hapa nimekupa mfano wa TANESCO na kirefu cha TANESCO na hakuna mtu aliyetafsiri kwamba TANESCO ni kifupi cha hilo nililokupa wewe. Kama ungekuwa hujui ukweli wa Shirika la TANESCO na mtu akakuwekea hivyo, wewe kama Mwanasheria, ungetafsiri hiyo entinty moja au entities mbili?
Johnson Mwanyika: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo sababu nasema kwamba inategemea, inawezekana mtu aliyeandika kwa kifupi alikosea.
Herbert Mtangi: Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine ni kwamba, hii Kamati imeundwa ndani ya Bunge na kwa bahati nzuri siku ile Spika anatamka, wewe kama AG ulikuwapo ndani ya Bunge. Kwa hiyo, unafahamu kuna mvutano katika mkataba wa Richmond unaozungumziwa hapa. Wewe kama AG, ambaye ndiye msimamizi mkuu katika kitengo kile, katika muda huo mfupi, umewahi kuusoma mkataba huu wa Richmond Development Corporation ambao ndiyo umeundiwa Tume?
Johnson Mwanyika: Mkataba huu niliupitia.
Herbert Mtangi: Kama umeupitia na wewe ni mtaalamu tena wa kubobea wa sheria, nini maoni yako katika mambo mawili; Je, unadhani Richmond ilishindwa kutekeleza mkataba au ilifanya uamuzi tu wa kawaida wa ku-assign kazi zake kwa Dowans?
Johnson Mwanyika: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine unapoambiwa toa ushauri wa kisheria, huwa tunaandikiwa na tunaulizwa maswali ambayo tunatakiwa tuyajibu. Kwa hiyo, hili nitakalozungumza hapa, linatokana na ufahamu wangu kuhusu suala hilo.Ninavyofahamu ni kwamba, kulikuwa na masharti ambayo yalikuwa yamewekwa kwenye ule mkataba. Sharti mojawapo ni kwamba, lazima Serikali ifungune Letter of Credit ili kuwawezesha Richmond kuleta hiyo mitambo. Hilo lilileta matatizo kidogo, Serikali ilichukua muda kidogo kufungua Letter of Credit, kwa sababu ilishindwa, hilo siwezi kulielewa, watu wa Nishati ndiyo wanaweza kujua zaidi kuliko mimi lakini nadhani mpaka mwisho ile Letter of Credit ilikuwa haijafunguliwa. Walipochukua watu wa Dowans ndipo Letter of Credit ikafunguliwa na mambo ndiyo yakaanza kuendelea vizuri, hivyo ndivyo ninavyofahamu.
Mohamed Habib Juma Mnyaa: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru. Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu, kwa vile umesema mkataba umeusoma na kwa kuwa wewe ndiye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mara nyingi sana katika mikataba kunakuwa na kipengele cha definitions na interpretations. Sasa ikiwa katika Mkataba huu kuna definition ya abbreviation RDECO halafu ikitafsiriwa kwamba, RDEVCO ni Richmond Development Corporation wakati abbreviation hiyo katika definition and interpretation haimo; je, itakubalika kisheria kwamba, hiyo RDEVCO ndiyo Richmond?
Johnson Mwanyika: Labda unipe huo Mkataba niuangalie, nione mahali ambapo una-refer.
Mohamed Habib Juma Mnyaa: Mkataba huu unazungumzia agreement ya emergency between Tanzania Electrical Supply Company na Richmond Development, lakini kwenye definition and interpretations, mimi sijaona hiyo definition au interpretation ya RDEVCO. Nikija katika minutes, kuna kitu kimetajwa RDEVCO, sasa ikiwa katika interpretation na definition hakuna tafsiri; je, nichukulie hii RDEVCO kuwa ndiyo Richmond Development Company?
Johnson Mwanyika: Mheshimiwa Mwenyekiti, lililokuwa referred kwenye minutes za vikao hivi, karibu watu wote waliohudhuria, mashirika waliyotoka yameandikwa in short form. Sasa tafsiri iliyotokana kwenye Mkataba ni kwa ajili ya mambo yaliyokuwa kwenye Mkataba wenyewe. Haya mambo yanayozungumzwa kwenye minutes ni minutes za kikao walichokaa hawa watalaamu wa haya mashirika ambayo yamekuwa represented kwenye kikao hiki.Ukiangalia hata watu wa TANESCO, haikuandikwa Tanzania Electrical Supply Company Limited imeandikwa TANESCO, watu wa CPI wameandikwa CPI, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wameandikwa AG, Benki Kuu wameandikwa Bank of Tanzania hawakuandikwa BoT, lakini hawa wengine ilikuwa ni short form ya makampuni wanayotoka.Sasa mimi kwa sababu nafahamu kwamba, huyu Gire ni mmoja wa wakurugenzi wa RDEVCO, nina hakika kwamba, iliyoandikwa RDEVCO ilikuwa ni hiyo kampuni inayozungumziwa kwenye mkataba. Hata ukiangalia kwenye Mkataba kwenye definition section, hakuna ambapo imeandikwa kwamba AG means what. Kwa haya yaliyozungumzwa hapa, mambo ya short form yalikuwa kwenye mikutano iliyofanyika wakati wa ku-negotiate huo mkataba.
Herbert Mtangi: Tukujazie hapo hapo, hebu tusaidie. Umeona Mkataba na minutes: Je, kwa utaalamu wako, kisheria minutes hizo zina form part of the contract?
Johnson Mwanyika: Inategemea watu walivyopatana, walivyoingia Mkataba walipatanaje kwamba hizi minutes ziwe sehemu ya Mkataba au namna gani. Kama walipatana kwamba ziwe sehemu ya Mkataba, inakuwa sehemu ya Mkataba na kama hawakupatana kuwa sehemu ya Mkataba haiwezi kuwa sehemu ya Mkataba. Maofisa ambao niliwatuma walisema kwamba, wakati wa ku-negotiate walikubaliana hizi minutes ziwe sehemu ya mkataba.
Herbert Mtangi: Je, hilo halikupaswa kuandikwa kwenye ule Mkataba wenyewe kwamba kuna minutes zitakuwa attached na zita-form part of the contract?
Johnson Mwanyika: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyofahamu, mara nyingi kuna mikataba mingine ya kuzungumza tu si lazima kila kitu mlichopatana kati yako wewe na mtu mwingine kiandikwe, vile vitu muhimu tu ndiyo vinavyoandikwa. Kama kwenye negotiations walikubaliana kwamba ile itakuwa part ya agreement ni kitu ambacho walipatana, basi.
Lucas Selelii: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwanasheria anaposema kwamba vitu muhimu ndivyo vinavyoandikwa, hivi ndani ya minutes humo kuna vitu muhimu sana kama kumhusisha Pratt and Whitney kwenye Mkataba kati ya Richmond na Pratt and Whitney, lakini ndani ya Mkataba Pratt and Whitney wala hawatajwi kabisa; haoni hicho nacho ni muhimu ingeandikwa kwamba minutes hizi ni part ya Mkataba?
Johnson Mwanyika: Mheshimiwa Mwenyekiti inawezekana labda kulikuwa na upungufu huo, lakini ukweli ni kwamba, yule ofisa ambaye alikuja mbele yenu hapa yeye alisisitiza kwamba, walikubaliana hizi minutes ziwe sehemu ya mkataba na yeye katika utaalamu wake wa kisheria anasema, wakati mwingine ndivyo inavyokuwa si lazima uziandike kwenye mkataba, alivyoeleza yeye.
Stella Manyanya: Unafikiria ni kitu gani pengine kinaweza kikawa kimesababisha huyu mwenzetu wa upande wa pili, kujiita jina ambalo halijaandikishwa popote kisheria lakini wakati huo huo, hata hayo makubaliano unayosema ameingia na huyu Pratt and Whitney amejiita kwa jina lile ambalo ameandikishwa; huoni kama alikuwa anacheza mchezo fulani hivi?
Johnson Mwanyika: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, mambo yote kuhusiana na huyo mtu kwamba alikuwa ni mtu gani, alitokea wapi, watu wa Nishati ndio wanaelewa vizuri zaidi. Ile timu ambayo ilizungumza na huyu mtu, ndiyo ingepaswa kujua huyu mtu alikosea wapi na ni nani na kwa sababu gani alitumia majina mawili tofauti.
Lucas Selelii: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwarudishe nyuma kidogo. Pamoja na kwamba watu wa Nishati na Madini ndio wanajua zaidi, nadhani atakumbuka kwamba, wakati ule wa dharura yeye AG, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, ndio walikuwa watu wa kwanza kupewa hili jukumu; haoni kwamba na yeye anahusika kwa kiwango kikubwa zaidi?
Johnson Mwanyika: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nakumbuka vizuri, katika kikao cha Baraza la Mawaziri cha tarehe 10 Februari, kilichosemwa ni kwamba, watakaosimamia hili zoezi la kutafuta hawa wakandarasi ni Wizara ya Nishati na Madini, ambayo Katibu Mkuu wake atakuwa Mwenyekiti halafu kukawa na wajumbe kutoka Wizara ya Fedha na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lakini ofisi yangu ilishirikishwa wakati wa ku-negotiate. Wakati wa kumtafuta huyu mtu, ni maofisa wale wengine kutoka Wizara nyingine ndio waliohusika, Ofisi ya AG ilihusishwa tu wakati wa ku-negotiate huu Mkataba, huo ndio ukweli.
Lucas Selelii: Lakini hapo hapo, taarifa ambazo tunazo, Ofisi ya Mwanasheria haikutajwa zaidi ya AG na Mwenyekiti alikuwa Katibu wa Wizara ya Fedha, ambao baadaye walikuja kuunda hiyo Steering Committee ikaja ikaunda hao unaowasema. Sasa mimi ninamrejesha hapo mwanzoni, kama Baraza la Mawaziri liliona yeye ni mtu muhimu kuhusika na hili jambo; kwa nini wanajitoa mara kwa mara kwamba hawahusiki?
Johnson Mwanyika: Napenda kurudia kusema kwamba, Baraza la Mawaziri lilisema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ndiyo imesemwa hivyo si kwa kukosea. Kwa sababu kama nilivyosema, mimi ndiye kiongozi wa ile ofisi lakini wakati wa kutafuta ushauri wa kisheria, si lazima iletwe moja kwa moja kwangu, inapelekwa kwa Law Officers. Law Officer ni mwanasheria yeyote ambaye ana cheo kinachozidi cha Senior State Attorney. Kwa hiyo, wizara yoyote inaweza kuomba ushauri kutoka kwetu kwa watu wa aina hiyo.Kama nilivyosema, kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu pia kuna Idara na kuna mtu anayeshughulika na mambo ya Civil and International ni Mkurugenzi wa Civil and International. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, anakutana na hivyo vitu wakati akicheki mafaili ambapo barua zilizoandikwa kwa wiki huwa humo, litapita kwangu nazicheki zote ndiyo najua mambo ambayo yanatendeka kwenye Wizara. Kiutendaji ni kwamba, wale Law Officers ndio ambao wanatoa ushauri kwa zile wizara, wakiomba kimaandishi kutoka kwenye wizara hizo.Inawezekana kweli kabisa labda kuna ofisa ambaye alihusishwa mwanzoni kabisa katika zoezi hilo, maana mimi ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuna Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ndiye Katibu Mkuu, yawezekana kabisa kwamba, kwa sababu ilikuwa ni Makatibu Wakuu ndio walisimamia zoezi hilo, yawezekana kabisa Katibu Mkuu wakati ule ambaye ni Mheshimiwa Limbu, labda alihusishwa kwenye zoezi hili la kwanza kabisa. Mimi kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali, niliteua mtu wakati wa ku-negotiate lakini tender ilikwendaje, watu wa Nishati ndio wanaojua zaidi.Mohamed
Habib Juma Mnyaa: Mheshimiwa Mwenyekiti, itabidi format ya maswali ibadilike kutokana na majibu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Mimi ninalotaka kuuliza, nakuuliza kama Mwanasheria Mkuu; Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu, Richmond ilikuja kwa sababu ya kuzalisha umeme wa dharura kwa kipindi ambacho Tanzania tulikuwa katika janga kubwa la kukosa umeme.Hivyo, ilitakiwa kuzalisha umeme katika kipindi cha miezi mitano, lakini ilishindwa badala yake imetumia miezi 16 hadi kutimiza zile megawatts 100. je, unaishauri nini Serikali ukizingatia kuwa, umuhimu ule wa dharura haupo tena na gharama Serikali ilizoingia ni mara mbili kwa umeme huu? Je, tuendelee nao tena kwa kipindi cha miaka miwii kuanzia Oktoba walipokamilisha au vipi? Unaishauri nini Serikali katika kipindi hiki ambapo udharura huo haupo tena?
Johnson Mwanyika: Mheshimiwa Mwenyekiti, tukio hilo linanipa matatizo kidogo kwa sababu hilo ni jambo ambalo linahitaji taaluma ya hao watu ambao wanahusika na mambo hayo. Ninavyofahamu, kuna Mkataba ambao Serikali iliingia na huyo Richmond ambao baadaye ulikuwa assigned kwa Dowans. Kwa hiyo, kama tulipatana kwamba huyu mtu alete mitambo hiyo akae kwa miaka miwili au mwaka mmoja, tukimwambia aondoke, tutakuwa tunavunja Mkataba ule.
Mohamed Habib Juma Mnyaa: Ikiwa pia tulikubaliana kwamba umeme wa dharura tunauhitaji kwa miezi mitano na hatukuupata kwa miezi mitano hii?
Johnson Mwanyika: Kama nilivyosema ni kwamba, yapo masharti yalikuwapo kwenye mkataba ambayo pia upande wa pili haukutekeleza na ndiyo sababu walishindwa kuleta hizi mashine mapema zaidi.
Dk. Harrison Mwakyembe: Waheshimiwa wabunge, nafikiri tumekaa kiasi cha kutosha na ratiba bado ni ndefu, naomba mniruhusu nichukue fursa hii kumshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa kuitikia wito wetu na kuja ili tuweze kubadilishana mawazo. Tunakuomba basi huyo Afisa wako Chidowu kama ukipita pale, mtaarifu tu kwamba, tutamuhitaji tena ili tuweze kufanya final touches sehemu ambazo nadhani yeye alitegemea AG ndiye atakuja kuzijazajaza, lakini kumbe ulishampa authority yote na tutakushuru sana ukimtaarifu.

No comments:

FEEDBACKS/RECOMMENDATIONS/SUGGESTIONS WRITE HERE

How did you hear about us?
Please give us your recommendations about our services in the space provided below.
Name:
Email Address:

create form

Mashauri Musimu

Mashauri Musimu
SOLICITOR-Ilala Municipal Council